Viongozi wanawake katika kaunti ya Kirinyaga wamelaani vikali kushambuliw na kujeruhiwa kwa mwakilishi wa wanawake wa kaunti hiyo Jane Njeri siku chache zilizopita.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa kundi la wawakilishi wadi wanawake katika bunge la kaunti ya Kirinyaga Milkah Thoithi, viongozi hao walisisitiza haja ya unyenyekevu na heshima miongoni mwao.
Wakizungumza katika majengo ya bunge hilo, viongozi hao kwa kauli moja waliwashutumu vijana wanaotumiwa na wanasiasa kushiriki maandamano ya vurugu.
Aidha walisisitiza haja ya kudumishwa kwa amani wakiitaja kuwa msingi wa mazingira bora ya utendakazi.
Waliongeza kuwa enzi ya siasa chafu ambapo wanasiasa walijihusisha na njama ya kuwadhulumu au kuwanyanyasa wapinzani wao ili kujizolea umaarufu imepitwa na wakati.
Badala yake, wanasema utoaji huduma bora kwa raia unapaswa kuwa msingi wa kujitafutia umaarufu.
Walitaja azima ya viongozi kuwania nyadhifa mbalimbali kuwa chanzo cha mafarakano ya kisiasa.
Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti ya Kirinyaga Jane Njeri alishambuliwa na kujeruhiwa wakati makabiliano makali yaliposhuhudiwa katika mji wa Kerugoya, kaunti ya Kirinyaga Agosti 22 baada ya uhasama kuzuka kati ya makundi mawili pinzani ya kisiasa.
Kizaazaa kilianza pale Njeri akiandamana na mwakilishi wadi wa Baragwi David Mathenge na wafuasi wao walipoandamana kuelekea ofisi za Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI tawi la Kerugoya kulaani madai dhidi ya Mathenge kwamba alifungua kisima cha Mukandu katika wadi ya Kanyekini kinyume cha sheria.
Vurugu zilianza wakati kundi linaloaminika kuwa la kambi pinzani lilipojitokeza na kukabiliana na lile la Mathenge.
Njeri tayari ameandikisha taarifa kuhusiana na kisa hicho huku uchunguzi ukiendelea kwa lengo la kuwawajibisha waliohusika.