Viongozi wahimiza wakazi wa Isiolo kuwa na umoja

Bruno Mutunga
3 Min Read
Gavana Abdi Guyo akiwasalimu wakazi wakati wa mkutano wa "Isiolo Pamoja"

Viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Isiolo wametoa wito wa kudumisha amani na kuvumiliana kisiasa kufuatia jaribio la kumwondoa mamlakani Gavana Abdi Guyo kupitia hoja ya kumng’atua, ambayo ilitupiliwa mbali na Seneti katika hatua za awali.

Katika mkutano wa hadhara uliopewa jina la “Isiolo Pamoja”, uliofanyika katika eneo la katikati mwa mji wa Isiolo hapo jana, viongozi hao wakiongozwa na Gavana wa sasa Abdi Ibrahim Guyo, Gavana wa kwanza wa kaunti hiyo Godana Doyo, na Mwakilishi wa Wanawake Mumina Bonaya, waliwahimiza wakazi wa Isiolo kudumisha umoja na kuepuka siasa za chuki na mgawanyiko wa kikabila zinazochochewa kwa maslahi ya kisiasa ya kibinafsi.

Gavana Guyo alisema kuwa hana kinyongo na yeyote aliyehusika katika jaribio la kumtimua, na akawataka viongozi wote kushirikiana naye katika kuhakikisha utoaji bora wa huduma kwa wananchi wa Isiolo katika kipindi kilichosalia cha uongozi wake.

Katika mabadiliko makubwa ya kisiasa, madiwani 10 kati ya 16 waliounga mkono hoja ya kumtimua sasa wamebadili msimamo na kutangaza kumuunga mkono Gavana Guyo.

Hatua hiyo imeimarisha wingi wake wa kura katika bunge la Kaunti, na kuiacha kambi pinzani na madiwani sita pekee. Hali hiyo huenda ikasaidia kutatua mvutano uliokuwepo bungeni, ambapo kulikuwa na mabunge mawili yaliyodai kuwa halali, pamoja na utata kuhusu nani ni Spika halali — Abdullahi Banticha ambaye sasa anaungwa mkono na madiwani 12, huku Mohamed Roba akiungwa mkono na madiwani 6 pekee. Bunge la kaunti ya Isiolo lina jumla ya madiwani 18.

Guyo alisema aliamua kutoandaa mkutano mara baada ya kunusurika jaribio hilo la kumng’atua ili kuepusha kuchochea zaidi mazingira ya kisiasa ambayo tayari yalikuwa na joto, kufuatia ushauri aliopewa na Spika wa Seneti, Amason Kingi, kwamba ajitahidi kupatanisha uhusiano wake na madiwani pamoja na viongozi wengine badala ya mikutano ya hadhara.

Kauli yake iliungwa mkono na Bonaya na Doyo, ambao waliwataka wakazi wa Isiolo kukataa siasa za chuki na badala yake kumpa Gavana Guyo nafasi ya kuwahudumia wananchi.

Doyo, ambaye alimaliza wa pili katika uchaguzi wa mwaka 2022 nyuma ya Guyo, pia alitangaza rasmi kumuunga mkono Gavana huyo, akisema sasa magavana wote watatu wa Isiolo – wa kwanza, wa pili na wa sasa – wanashirikiana kwa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa kaunti hiyo.

Kwa upande wake, Bonaya alisema kuwa wananchi wa Isiolo wamepoteza zaidi ya miezi miwili katika siasa zisizo na umuhimu, na sasa ni wakati wa kufanya kazi hadi pale kampeni rasmi za uchaguzi wa 2027 zitakapoanza.

Viongozi hao pia walionyesha kuunga mkono serikali ya Rais William Ruto, wakisema kuwa amekuwa mstari wa mbele kuwaletea maendeleo wakazi wa Isiolo na Kaskazini mwa Kenya kwa jumla.

Bruno Mutunga
+ posts
Share This Article