Viongozi wa serikali tatu za kijeshi za Afrika Magharibi, wanatarajiwa kukutana pamoja kwa mara ya kwanza ili kuimarisha muungano ulioundwa kutokana na upinzani kutoka nchi jirani.
Wanajeshi hao walichukua mamlaka nchini Mali, Burkina Faso na Niger katika mfululizo wa mapinduzi kutoka 2020 hadi 2023.
Nchi zote tatu – ambazo sasa zinaunda Muungano wa Mataifa ya Sahel – zimeathiriwa na ghasia za wanamgambo wa jihadi, ikiwa ni moja ya sababu iliyotolewa kwa jeshi kuchukua mamlaka.
Mnamo Januari, wote walitangaza mpango wa kuondoka katika Jumuiya ya Kikanda ya Ecowas, ambayo inashikilia mkutano wake wa kilele siku ya Jumapili.
Katika mkutano wa Jumamosi katika mji mkuu wa Niger, Niamey, wakuu hao wa serikali za kijeshi wanatarajiwa kuanzisha rasmi muungano huo, unaojulikana kwa kifupi kwa lugha ya Kifaransa kama AES.
Nchi zote tatu zimewafukuza wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa pale kama sehemu ya ujumbe wa kupambana na jihadi na kuigeukia Urusi kwa usaidizi wa kijeshi.