Viongozi wa Kwale wakutana kujadili masuala ya ardhi ili kuvutia wawekezaji

Mkutano huo ulilenga kujadili mizozo ya ardhi ambayo inakwamisha uwekezaji.

Marion Bosire
3 Min Read
Gavana wa Kwale Fatuma Achani.

Viongozi wa kaunti ya Kwale wakiongozwa na Waziri anayeondoka wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji Salim Mvura na Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani, walifanya mkutano wa ngazi za juu katika Kituo cha Utamaduni cha Kwale kilichopo katika kaunti ndogo ya Matuga, kujadili mizozo ya ardhi ambayo inakwamisha uwekezaji.

Mkutano huo ulilenga kuleta pamoja viongozi wa Kaunti wakiwemo wabunge wanne wa maeneo ya Kinango, Msambweni, Matuga na Lungalunga pamoja na Wajumbe wa Bunge la Kaunti, wakiungana na Spika wa Kaunti, Seth Mwatela Kamanza.

Baadhi ya maeneo yanayokumbwa na mizozo ya ardhi katika Kaunti ya Kwale ni pamoja na Lungalunga, Mwereni, Chanze, Caslank na Kidomaya.

Akizungumza katika mkutano huo, Mvurya alisema kuwa kutokana na migogoro ya ardhi inayoshuhudiwa katika sehemu mbalimbali za Kaunti, wawekezaji wamekuwa wakiogopa kuwekeza huko.

Mvurya alisema ukosefu wa ardhi ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji umeleta changamoto ya ukosefu wa ajira kwa wakazi wa Kaunti ya Kwale na aliwataka viongozi kuungana kutafuta suluhisho la kudumu kwa tatizo hili.

“Tuna maeneo 39 ya maalum ya uchumi (SEZ) kote nchini ambayo tayari yamepangwa, pamoja na maeneo ya Uzalishaji wa Bidhaa kwa ajili ya Usafirishaji (EPZ) ambapo tumetambua maeneo 7 kwa ajili ya kuanzishwa kwa vituo hivyo,” alisema Mvurya.

Kwa upande wake, Gavana Fatuma Achani alisema utawala wake unashirikiana kwa karibu na Serikali ya Taifa na taasisi mbalimbali kama Tume ya Maadili na Kupambana na Rushwa (EACC) kuhakikisha kuwa inaunda mazingira bora ya uwekezaji na kutatua mizozo ya ardhi katika Kaunti.

“Hakuna njia ambayo Gavana anaweza kufanya maamuzi binafsi kwa ajili ya Kaunti, ndio maana tumekusanyika hapa katika jukwaa hili kuona jinsi tunavyoweza kutatua masuala ya ardhi kama Kaunti,” alisema Achani.

Wajumbe wa Bunge la Kaunti wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati ya ardhi, Dawa Ngome, walisifia hatua ya viongozi kukutana wakisema mizozo ya ardhi itatatuliwa kupitia juhudi za pamoja.

“Mizozo ya ardhi imekuwa changamoto kwa muda mrefu, lakini natumai kuwa kwa mkutano huu tutapata suluhu,” alisema Dawa.

Wakati wa ziara yake ya maendeleo katika eneo la Pwani mwaka huu, Rais William Ruto aliahidi kutoa shilingi bilioni moja za kununua ardhi kutoka kwa wamiliki wasioonekana na kuhamisha wakazi waliokosa makazi.

Kupitia juhudi za pamoja kati ya Kaunti za Pwani na Serikali ya Taifa, mizozo ya ardhi inaweza kuwa hadithi ya zamani.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *