Siku chache baada ya Naibu Gavana wa kaunti ya Trans Nzoia Philomena Kapkory kufika mbele ya kamati ya ugatuzi katika bunge la Seneti kuelezea wasiwasi juu ya uhusiano wake na Gavana George Natembeya, viongozi wa kidini katika kaunti hiyo wanataka wawili hao kupatanishwa.
Kadhalikaa wamewataka wawakilishi wadi wa bunge la kaunti hiyo kushirikiana na gavana kuwahudumia wakazi na kuacha migogoro na malumbano ambayo inahujumu maendeleo.
Kauli hii inajiri baada ya wakilishi wadi kuwasilisha notisi kwenye bunge ya kutaka kuwatimua baadhi ya maafisa wa kaunti kwa tuhuma za ufisadi na ukiukaji wa sheria, hali ambayo viongozi wa kidini wanahofia huenda ikawa kizingiti kikubwa kwa matunda ya maendeleo ambayo yameanza kushuhudiwa.
Wakiongozwa na Askofu Martin Mafumbo, wanasema uongozi uliopita ulikosa kufanikisha ajenda za maendeleo kutokana na malumbano ya aina hii ambayo yamechipuka.
Wanawataka wawakilishi wadi 27 ambao tayari wametia saini kuunga mkono kubanduliwa kwa maafisa wa kaunti kutafuta njia mwafaka kutatua changamoto na lalama ambazo zimeibuliwa.