Viongozi wa kamati za bunge wasiohudhuria vikao waonywa

Marion Bosire
2 Min Read

Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah ametoa onyo kali kwa wenyeviti na manaibu wenyeviti wa kamati za bunge akisema kwamba kutohudhuria vikao vya bunge mara kwa mara huenda kukawasababishia kubanduliwa.

Onyo hili linajiri kufuatia kukosekana bungeni kwa wabunge ambao maswali yao yameratibiwa kujibiwa na mawaziri.

Ichung’wah alisisitiza kwamba ikitizamiwa kwamba kuna wenyeviti na manaibu wenyeviti wapatao 60, suala la akidi halifai kuwa tatizo katia bunge la taifa.

Akirejelea kifungu nambari 121 cha katiba ambacho kinasema kwamba akidi ni wabunge 50 na maseneta 15, Ichung’wah alisisitiza umuhimu wa kuhudhuria vikao kila mara.

Kulingana naye, viongozi wa kamati za bunge wanatosha kutimiza hitaji hilo iwapo wanatekeleza majukumu yao.

Bunge liliporejelea vikao vyake baada ya mapumziko ya mwezi mmoja, naibu spika Gladys Boss Shollei aliagiza kengele ya akidi ikirizwe kwa sababu ya ukosefu wa idadi hitajika ya wabunge.

Ichung’wah alikumbusha viongozi wa kamati mbali mbali kuhusu jukumu lao akisema walihudhuria mkutano wa viongozi wa bunge wiki jana ambapo suala la kuhudhuria vikao kwa upande wa viongozi liliibuliwa.

“Ikiwa wewe ni mwenyekiti au naibu mwenyekiti, ni lazima uwe bungeni saa nane unusu. Spika hafai kusubiri akidi itimie kwa sababu ya wabunge wasiotaka kuhudhuria vikao hasa wale wa kuongoza mijadala na kujibu maswali.” Alisema Ichung’wah.

Alihimiza wabunge wawe wakihudhuria vikao akisema iwapo hawana muda huo, basi wanafaa kuchukua hatua faafu akirejelea usemi wa Junet Mohamed kwamba huu ni msimu wa kubandua viongozi mamlakani.

“Sipendekezi kubanduliwa mamlakani kwa viongozi, lakini wanaotelekeza majukumu yao huenda wakakabiliwa na hilo.” alisema Ichung’wah.

Katika mkutano wa viongozi wa bunge la taifa huko Naivasha wiki jana, Spika Moses Masika Wetang’ula naye alionya viongozi wa kamati za bunge dhidi ya kukosa kuhudhuria vikao akisisitiza hatua hiyo muhimu kwa mipango ya bunge.

Website |  + posts
Share This Article