Viongozi na wadau wakusanyika shuleni Nkareta kusherehekea matokeo mazuri

2 Min Read

Baada ya kuandikisha matokeo mazuri katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE mwaka jana, viongozi wa kaunti ya Narok walikongamana katika shule ya upili ya Nkareta kusherehekea.

Alama ya wastani ya shule hiyo ni 8.3 na hivyo ikawa shule bora zaidi katika kaunti huku wanafunzi zaidi ya 62 wakipata alama ya C+ na zaidi.

Katibu wa masuala ya elimu katika serikali ya kaunti ya Narok Maiyani Tuya alipongeza usimamizi wa shule hiyo kwa matokeo mazuri huku akiahidi kutatua baadhi ya changamoto shuleni humo kama vile maji ya chumvi.

Mbunge wa eneo hilo la Narok Kaskazini Agnes Pareiyo Tuya naye aliahidi kuisaidia shule hiyo huku akiitaka iboreshe matokeo hata zaidi. Alihimiza waliofanya mtigani wa KCSE mwaka jana shuleni humo wajisajili kwa kozi za uuguzi ambazo kulingana naye zina fursa nyingi za ajira nchini Ujerumani.

Alifichua kwamba hazina ya kustawisha eneo bunge lake CDF ilisambaza zaidi ya shilingi laki 6 za usaidizi wa masomo kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Pareiyo aliahidi kujengea wanafunzi wa kiume bweni huku akitoa mchango wa shilingi milioni moja kama zawadi kwa shule hiyo kwa kufanya vyema.

Naibu Kamishna wa kaunti wa eneo la Narok ya kati Faith Mule ambaye pia alihudhuria mkutano huo alihimiza ushirikiano kati ya wadau wa elimu ili kuafikia asilimia 100 ya mpito kutoka kiwango kimoja cha elimu hadi kingine.

Mule alilalamikia mimba za mapema akisema wazazi, walimu, serikali ya kaunti na ile ya kitaifa sharti washirikiane ili kuhakikisha watoto wa kike wanasalia shuleni.

Alionya pia dhidi ya ukeketaji wa wasichana akisema lazima wazazi wawe waangalifu.

Waziri wa elimu wa serikali ya kaunti ya Narok Robert Simotwo alitoa changamoto kwa wanafunzi kuendelea kufanya vyema kwenye masomo ili kuimarisha matokeo ya watangulizi wao.

George Kuluo mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Nkareta aliomba majengo zaidi shuleni humo ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi wanaozidi kuongezeka.

Website |  + posts
Stanley Mbugua
Share This Article