Viongozi Lamu wapinga mswada wa kudhibiti shughuli za kidini

radiotaifa
1 Min Read

Viongozi wa kidini katika kaunti ya Lamu wamepinga vikali mswada unaopendekezwa wa kudhibiti shughuli za kidini na ibada, unaotarajiwa kuwasilishwa Bungeni hivi karibuni.

Viongozi hao wanahoji kuwa baadhi ya vipengele katika rasimu ya sheria hiyo vinaweza kufungua mlango wa matumizi mabaya ya rasilimali za umma. Pia wanadai kuwa viongozi wengi wa kidini na wakaazi wa eneo hilo wanasalia kutojua yaliyomo kwenye mswada huo, na hivyo kuibua wasiwasi kuhusu uwazi na ushirikishwaji wa umma.

Wakizungumza baada ya mkutano wa uhamasishaji kuhusu sheria inayopendekezwa, viongozi hao walikashifu kile walichokitaja kuwa kushindwa kukusanya maoni ya kutosha kutoka kwa washikadau wa Lamu na mikoa mingine, inavyotakikana kwa mujibu wa Katiba. Walishikilia kwamba ushirikishwaji wa umma wenye maana ni muhimu kabla ya sheria yoyote kama hiyo kujadiliwa Bungeni.

Sambamba na hayo, viongozi hao wameitaka serikali kuruhusu taasisi za kidini kujiendesha zenyewe. Wamedokeza matamshi ya awali ya Rais William Ruto yanayounga mkono kujidhibiti wakati wa mjadala kuhusu mswada wa awali uliofadhiliwa na Seneta wa Tana River Danson Mungatana.

Share This Article