Rais William Ruto amehimiza viongozi ambao ni vijana barubaru katika chama tawala UDA kuwa na subira wakati wao utafika.
Kiongozi wa nchi aliyasema hayo wakati wa ibada ya dhehebu la Akorino katika kaunti ya Nakuru ambapo pia aliahidi kwamba atakuwa kielelezo kwa viongozi hao wa umri mdogo na kuwapa ushauri.
Haya yanajiri wakati ambapo migawanyiko imeshuhudiwa katika chama tawala ambapo naibu rais Rigathi Gachagua anadai kwamba watu walio karibu na rais wanaingilia siasa za eneo la mlima Kenya.
Wakati huo huo Rais Ruto alihimiza viongozi kuwa na umoja wanapohudumia wakenya kwani ukosefu wa umoja huenda ukasababisha kutoelewana na hatimaye kuhujumu maendeleo nchini.
Ruto alisema Kenya ni kielelezo cha amani na utulivu ndiposa imeaminiwa na oparesheni za kuleta amani katika kanda hii na hata kimataifa.
Naibu rais alimhakikishia rais kwamba ataendelea kumuunga mkono na hatayumbishwa.