Viongozi 15 wa serikali kuhudhuria mikutano ya ngazi za juu Nairobi

Tom Mathinji
1 Min Read

Kenya itakuwa mwenyeji wa marais na viongozi wa serikali wapatao 15 na mawaziri 50 wa mashauri ya nchi za kigeni kwa mikutano ya ngazi za juu.

Kwenye taarifa, Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Alfred Mutua alisema mkutano huo wa tano wa  katikati ya mwaka wa ushirikishi unatarajiwa kuwahusisha wajumbe zaidi ya 1,500 kutoka kote barani Afrika.

Alisema wajumbe hao watahudhuria mkutano huo wa mpango wa ushirikishi unaotarajiwa kuandaliwa kati ya Julai 13 na 16 jijini Nairobi.

Mpango huo ulianzishwa mnamo mwaka  2017 kama kitengo maalum cha Tume ya Umoja wa Afrika, mashirika ya kiuchumi Barani na mipango ya kanda ya kulainisha utendakazi na kushirikisha utekelezwaji wa ajenda ya utangamano ya bara Afrika.

Mkutano wa marais na viogozi wa serikali utafanyika Julai 16 katika makao ya Umoja wa Mataifa huko Gigiri, jijini Nairobi.

Mkutano wa tano wa ushirikishi utatanguliwa na Kikao cha 43 cha Kawaida cha Baraza Kuu la Umoja wa Afrika, ambalo linawaleta pamoja mawaziri wa mambo ya nje kutoka barani.

Mawaziri hao watazingatia na kupitisha bajeti ya fedha ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2024, kutathmini utekelezaji wa maamuzi ya umoja huo na kupitisha maamuzi mapya kuhusu masuala muhimu kuhusu bara afrika miongoni mwa mengine.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *