Mshambulizi wa Real Madrid na Brazil Vinicius Junior na Aitana Bonmati wa Barcelona na Uhispania, ndio wachezaji bora wa mwaka huu katika tuzo za Shirikisho la Soka Duniani, FIFA.
Vinicius alitangazwa mshindi katika sherehe zilizoandaliwa jana usiku mjini Doha, Qatar.
Nyota huyo wa Brazil alishinda tuzo hiyo kwa mara ya kwanza na pia alikuwa amemaliza wa pili katika tuzo ya Ballon D’or iliyotwaliwa na Rodri wa Uhispania.
Vinicius alipata asilimia 48 ya kura zilizopigwa na makocha, makapteni na wanahabari kutoka mataifa yote wanachama wa FIFA.
Rodri alimaliza wa pili kwa asilimia 43 huku Jude Bellingham akipata asilimia 37.
Tuzo ya wanawake ilinyakuliwa na Bonmati kwa asilimia 52 ,akifuatwa na Barbra Banda wa Zambia kwa asilimia 39.
Carlo Ancelloti wa Real Madrid alishinda tuzo ya kocha bora wa mwaka akifuatwa na Xabi Alonso wa Bayer Leverkusen.
Emiliano Martinez wa Aston Villa na Argentina alinyakua tuzo ya kipa bora wa mwaka.