Vikosi vya usalama vyarejesha utulivu kaunti ya Tana River

Tom Mathinji
1 Min Read
Mrakibu wa eneo la Pwani Rhoda Onyancha.

Vitengo vya usalama kanda ya Pwani vimeimarisha juhudi za kurejesha hali ya utulivu katika kaunti ndogo za Bangale na Tana Kaskazini, kaunti ya Tana River. Hii inafuatia mzozo kati ya jamii za eneo hilo uliosababisha vifo vya watu wanane.

Akihutubia wanahabari katika afisi ya Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Bangale, mratibu wa eneo la Pwani Rhoda Onyancha alisema maafisa wa usalama wamekita kambi katika maeneo yanayokumbwa na mzozo ili kudumisha usalama.

Onyancha, aliyekuwa ameandamana na kundi la maafisa wa usalama, alisema ni jambo la kusikitisha kwamba maisha yanapotea kufuatia ghasia kati ya jamii mbili ambazo zimeishi pamoja kwa muda mrefu.

“Tumejaribu kubainisha chanzo halisi cha mzozo huo, na tumegundua kwamba kulikuwa na mtafaruku katika kituo cha maji cha Anole, ambapo jamii moja ilihisi kuzuiliwa kutumia maji hayo,” alisema Onyancha.

Alitoa wito kwa wazee wa jamii hizo kushiriki mazungumzo wakati wa kutatua migogoro, na iwapo watashindwa kupata suluhu, wawaalike wazee wa jamii nyingine kuhakikisha maswala yanatatuliwa na hayaenei zaidi.

Onyancha aliwahimiza wazee wa jamii hizo kushirikiana na maafisa wa usalama kukabiliana na silaha haramu mikononi mwa raia, akionya kuwa zoezi la kutwaa silaha haramu litatekelezwa iwapo hazitasalimishwa kwa hiari.

Website |  + posts
Share This Article