Vijiji kadhaa vyasalia mahame kaunti ya Tana River

Tom Mathinji
1 Min Read
Wakazi watoroka makwao kufuatia utovu wa usalama Tana River.

Vijiji kadhaa katika kaunti ndogo za Bangale na Tana kaskazini, vimesalia mahame, baada ya wakazi kutoroka kutokana na hali ya utovu wa usalama inayoshuhudiwa katika eneo hilo.

Watu wanne zaidi waliuawa siku ya Jumamosi na watu waliokuwa wamejihami katika eneo la Meti, Tana kaskazini na kufikisha 18  idadi ya watu waliouawa tangu ghasia hizo kuzuka juma lililopita.

Wiki iliyopita wavamizi walimuua mwana wa chifu wa Nanigi Mohamed Ramadhani Hiribae, wakateketeza nyumba yake na ile ya naibu wake Bajila Mohamed.

Nyumba kadhaa katika maeneo hayo yameteketezwa, katika mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Siku ya Ijumaa waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki, aliweka kafyu ya siku 30 katika maeneo 12 yaliyoko kaunti ndogo za Bangale na Tana Kaskazini, akiyataja hatari na yasio na usalama.

Wakati huo huo, Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja, aliwaagiza wakazi wote wa maeneo hayo kusalimisha silaha zote wanazomiliki katika vituo vya polisi vilivyo karibu.

Share This Article