Vijana watatu wakamatwa kwa kuhusika na utekaji nyara bandia

Tom Mathinji
2 Min Read

Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI  katika eneo la Imenti Kaskazini, Kaunti ya Meru, wamewakamata vijana watatu waliohusika na kisa bandia cha utekaji nyara.

Watatu hao, wote wenye umri wa miaka 17, walilenga kujipatia shilingi milioni sita kutoka kwa familia moja ya vijana hao.

Njama hiyo ilianzia Kainginyo, Thimbiri, wakati washukiwa wawili wa kiume na mmoja wa kike, anayedaiwa kuwa mwathiriwa, walipanga mpango wa kuripoti utekaji bandia nyara wake.

Kulingana na idara ya upelelezi wa jinai (DCI), njama ya watatu hao ni pamoja na kughushi utekaji nyara ili kulipwa ridhaa.

Kisha kundi hilo lilidai pesa kutoka kwa wazazi wake, na kuonya kwamba binti yao angetoweka kabisa ikiwa kiasi kikubwa cha pesa hakitalipwa.

Kulingana na polisi, wakiwa na hofu kubwa, familia hiyo ilijaribu kuzungumza na waliodhaniwa kuwa watekaji nyara, lakini jitihada zao hazikufaulu.

Kufuatia uchunguzi wa kitaalamu, serikali iliwasaka vijana hao hadi mafichoni huko Kainginyo, ambako walikamatwa.

Wakati wa msako huo, wapelelezi walisema waligundua misokoto 20 ya bangi katika eneo walimokuwa vijana hao.

Huku familia ikiwa imefarijika kwa kuwa binti yao yuko salama salmin, vijana hao watatu sasa wako kizuizini katika Kituo cha Polisi cha Igoji wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kupanga njama za kulaghai na kupatikana na mihadarati.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article