Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi ametoa wito kwa vijana wanaofanya kazi katika mataifa ya ughaibuni kudumisha nidhamu, kutii sheria za mataifa hayo na kueneza sifa nzuri za taifa hili.
Mudavadi aliyepia waziri wa Mambo ya Nje, alisema Kenya inajivunia jina zuri kote ulimwenguni, hivyo vijana wanaoelekea katika mataifa ya kigeni kufanya kazi wanajukumu la kudumisha na kutetea sifa nzuri ya Kenya.
Akizungumza alipofungua rasmi maonyesho ya ajira, kuadhimisha miaka 60 ya Kenya kuhusu masuala ya kidiplomasia, Mudavadi alisema nidhamu ni muhimu kwa vijana hao ili wasije wakajipata taabani katika mataifa wanakohudumu.
“Mnapotua katika nchi ya kigeni, sheria za taifa hilo zinaanza kufanya kazi. Ikiwa umezoea kutozingatia sheria hapa nchini, utapata changamoto ughaibuni. Heshimu sheria za mataifa hayo na uwakilishe Kenya kwa heshima,” alisema Mudavadi.
Alisisitiza kwamba sifa njema ya Kenya katika mataifa ya kigeni huwa na manufaa makubwa kuwavutia wawekezaji.
Mudavadi aliyepia kaimu waziri wa usalama wa taifa alionya dhidi ya mienendo isiyofaa miongoni mwa wakenya wanaoenda kufanya kazi ughaibuni, akikariri umuhimu wa kuheshimu sheria.
Alisisitiza kuwa nidhamu ni nguzo muhimu ya kuwavutia wawekezaji nchini Kenya, akidokeza kuwa tabia za wakenya ughaibuni zitaangazia taswwira nzuri ya taifa hili na kukaribisha wawekezaji.