Vijana wahimizwa kutumia mitandao kujipatia riziki

Tom Mathinji
1 Min Read
Tessie Mudavadi.

Mkewe waziri mwenye mamlaka makuu Tessie Mudavadi, ametoa wito kwa vijana hapa nchini kutumia ipasavyo majukwaa ya mitandao kufanya shughuli za kibiashara, kubuni nafasi za kazi na uzalishaji wa mali kwa ajili ya ukuaji wa kiuchumi wa taifa hili.

Bi. Mudavadi alisema kwamba ijapokuwa mitandao ya kijamii inatumiwa kwa ajili ya habari na burudani, pia inaweza kuwasaidia wataalamu wa teknolojia kubuni na kukuza masoko ili bidhaa zinazozalishwa humu nchini zilete kipato.

Akizungumza Nakuru wakati wa uzinduzi wa mpango wa Ushirika Wema uliowaleta pamoja zaidi ya vijana 1,000 wajasiriamali kutoka kaunti ya Nakuru, Tessi alisema kwamba vijana ni washiriki muhimu katika azma ya Kenya ya kuwa na uchumi wa kipato cha wastani ifikapo mwaka 2030.

Aidha aliongeza kuwa uvumbuzi pamoja na matumizi ya mtandao ni nguzo kuu kuafikia lengo hilo

Akiunga mkono kauli zake, waziri wa biashara, vyama vya ushirika na mikopo pamoja na utalii katika kaunti ya Nakuru Stephen Kuria, aliwashauri vijana kutumia fursa ya vifaa vya biashara vilivyotolewa na serikali ya kaunti ili kuimarisha maisha yao.

Kuria aliongeza kuwa serikali ya kaunti ya Nakuru imetenga shilingi milioni 100 katika mwaka huu wa kifedha ili kupiga jeki biashara zinazoanzishwa na vijana pamoja na wanawake katika kaunti hiyo

Share This Article