Naibu Rais Rigathi Gachaua amesema serikali imewasikiliza vijana, huku akiwahimiza waipe serikali muda kutekeleza matakwa yao.
Akizungumza leo Jumamosi alipohudhuria ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Samuel Kirimi Julius na wahudumu 33 wa kanisa la Mwea, PEFA Cathedral, naibu huyo wa Rais aliwataka vijana kusitisha maandamano kwa kuwa wahuni wameteka nyara maandamano na kusababisha vurugu.
Aidha Gachagua alielezea kujitolea kwa serikali kuwahudumia wakenya na kuendelea kushirikiana na wote katika kufanikisha ajenda ya maendeleo.
Naibu huyo wa Rais alisema licha ya changamoto zinazoshuhudiwa hapa nchini, zilizoko, serikali imewaajiri walimu 56,000, katika kipindi cha mwaka mmoja akiongeza kuwa Rais William Ruto amefanikiwa kudhibiti gharama ya juu ya maisha hapa nchini.
Naibu Rais alifichua kuwa serikali inanuia kufutilia mbali madeni yanayodaiwa vyama vya ushirika vya kahawa, akisema marekebisho yaliyofanywa, yameanza kuleta manufaa.
Akizungumza katika hafla hiyo, mke wa Naibu Rais Dorcas Rigathi, alitoa wito kwa kanisa kuwa ujasiri, huku serikali ikiendelea kuwahudumia wananchi.
Dorcas aliitaka kanisa kupaza sauti yake, hususan kuhusu utumizi wa dawa za kulevya na mihadarati.