Vijana wa Wiper wataka Odinga amwombe msamaha Kalonzo

Marion Bosire
1 Min Read
Kalonzo Musyoka akihutubu katika kanisa Katoliki

Baadhi ya vijana wanachama wa chama cha Wiper katika kaunti za Makueni, Machakos na Kitui sasa wanamtaka kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amwombe msamaha kiongozi wa chama chao Kalonzo Musyoka hadharani.

Haya yanajiri baada ya kile vijana hao wanakitaja kuwa kitendo cha kumkosea heshima kiongozi wao kilichotokea katika afisi za wakfu wa jaramogi Oginga ambapo hotuba ya Kalonzo ilikatizwa na wahuni.

Wakizungumza huko Machakos baada ya mkutano wa vijana wa chama cha Wiper, vijana hao walimtaka waziri mkuu wa zamani Raila Odinga aombe msamaha kwani Kalonzo amekuwa mwaminifu kwa Raila Odinga kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Huku wakisema kwamba Kalonzo anafaa kuheshimiwa na vyama tanzu vya muungano wa Azimio, vijana hao wametishia kushinikiza kuondolewa kwa chama cha Wiper kwenye muungano huo wa Azimio iwapo chaguo lake la kutounga mkono uundaji wa serikali inayojumuisha upinzani halitaheshimiwa.

Vijana hao wametaja hatua ya serikali kutaka kujumuisha upinzani uongozini kama usaliti kwa wakenya na hasa vijana wa Gen Z ambao wamekuwa wakiandamana kushinikiza utawala bora.

Siku chache zilizopita, mkutano wa viongozi wa muungano wa Azimio wakiongozwa na Kalonzo na wanahabari katika makao makuu ya wakfu wa Jaramogi Oginga ulisambaratishwa na wahuni dakika chahe baada ya kiongozi wa ODM kuondoka.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *