Vijana 90 wapatiwa vifaa vya kazi Makueni

Marion Bosire
1 Min Read

Vijana wapatao 90 kutoka sehemu mbali mbali za kaunti ya Makueni, wamepatiwa vifaa vya kufanyia kazi na naibu gavana wa kaunti hiyo Lucy Mulili, ili waanzishe biashara zao.

Tisini hao wamekuwa wakipokea mafunzo kwa muda wa wiki nane zilizopita kuhusu kazi mbali mbali za mikono chini ya uangalizi wa wataalamu kwenye mpango uliopatiwa jina la “Ujuzi teke Teke”.

Mpango huo ulianzishwa na idara ya jinsia, watoto, vijana, michezo na huduma kwa jamii.

Kulingana na mwanachama wa kamati kuu ya kaunti anayehusika na masuala ya jinsia mhandisi Peter Mumo, mpango huo unalenga kuziba pengo la ukosefu wa mtaji wa kuanzisha biashara kati ya vijana.

Naibu Gavana Mulili aliongoza shughuli ya utoaji wa vifaa hivyo katika taasisi ya pamoja ya mafunzo ya kiufundi ya Makueni iliyoko mjini Wote.

Alisema kwamba serikali ya kaunti ya Makueni, inalenga kuhakikisha uwepo wa watu wengi walio na ujuzi katika fani mbali mbali ambao wataendesha uchumi wa kaunti kupitia kujiajiri.

Share This Article