Kamati ya elimu na michezo katika bunge la taifa la Uganda imependekeza vigezo vipya kwa kila mwalimu nchini humo katika viwango vya chekechea, shule za msingi na shule za upili.
Walimu hao wanahitajika kuwa na shahada ya masuala ya elimu au nyingine husika pamoja na cheti cha diploma ili kusajiliwa.
Pendekezo hilo liko kwenye ripoti ya mswada wa kitaifa wa walimu wa mwaka 2023 iliyosomwa bungeni na mwenyekiti wa kamati hiyo ya elimu James Kubeketerya.
Kamati hiyo inasema mswada huo unakusudiwa kuhalalisha na kusanifisha taaluma ya ualimu nchini Uganda na mojawapo ya njia za kufanikisha hilo ni kuwataka wawe na digrii.
Mswada huo unapendekeza pia kubuniwa kwa baraza la kitaifa la walimu ambalo wanachama wake wanapendekezwa kuwa wataalamu katika sekta ya ualimu.
Wabunge wanapendekeza kwamba mswada huo uidhinishe ushirikiano kati ya baraza hilo la kitaifa la walimu na mashirika mengine ya sekta ya elimu kama kituo cha kuandaa mitaala.
Ushirikiano kama huo utatoa fursa ya juhudi za pamoja za kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa masomo ya mwendelezo ya walimu.
Kamati hiyo ya elimu ilikataa pendekezo la kipindi cha mwaka mmoja cha uanagenzi kwa walimu ikisema kwamba muda huo ni mrefu mno ikitizamiwa kwamba walimu hupata uzoefu wa kufundisha kama sehemu ya kozi zao.