Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Uganda Bebe Cool ametangaza ujio wa video ya wimbo wake mpya uitwao ‘Circumference’, Jumatano, Januari 8, 2025.
Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, Cool ambaye jina lake halisi ni Musa Ssali aliahidi kuonyesha wapenzi wa muziki wake matukio ya maandalizi ya video hiyo pia.
Wimbo huo ambao alitoa kwa umma kwa mara ya kwanza Disemba 13, 2024, ndio wa kwanza kwenye albamu yake ambayo anashughulikia kwa jina ‘Break the Chains’.
Bebe Cool anayetambuliwa na wengi kama mwanamuziki wa mtindo wa ragga, alianza kazi kama mwanamuziki mwaka 1997 jijini Nairobi, nchini Kenya, kabla ya kurejea Uganda.
Wakati huo alikuwa chini ya usimamizi wa kampuni ya kusimamia wanamuziki ya Kenya Ogopa Djs, ambayo pia ilikuwa inasimamia wasanii kama Redsan na Chameleone.
Katika kibao hicho cha ‘Circumference, Bebe Cool ametumia mtindo wa Afrobeat unaovuma sana lakini wapo ambao wanahisi kwamba angesalia kwenye mtindo wake wa awali.
Ana albamu alizozindua awali kama vile ‘Maisha’ na ‘Senta’ ambapo ametumia lugha tatu ambazo ni Kiswahili, Kiingereza na lugha ya Luganda.