VDM asema hayuko tayari kwa mapatano na Mercy Chinwo

Shirika moja la kidini limependekeza mapatano kati ya wawili hao badala ya kesi kortini.

Marion Bosire
2 Min Read
VDM

Mkosoaji wa mitandaoni nchini Nigeria Martins Otse maarufu kama Very Dark Man – VDM amebadili msimamo katika zogo linaloendelea kati yake na mwimbaji wa nyimbo za injili Mercy Chinwo.

Akijibu wito wa mapatano uliotolewa na shirika moja la kidini liitwalo Pentecostal Fellowship of Nigeria (PFN), VDM alisema hataki mapatano nje ya mahakama.

PFN ilikuwa imeomba wawili hao wasuluhishe tofauti zao badala ya kuendeleza kesi iliyowasilishwa mahakamani na Chinwo, ikisema kwamba iwapo itaendelea, itaharibu kabisa sura ya tasnia ya nyimbo za injili.

VDM amesisitiza kwamb anataka kesi hiyo iendelee kwani itafichua watesi pamoja na maovu katika idara ya mahakama.

Mkosoaji huyo alijipata matatani baada ya kutoa maoni yake kuhusu mzozo kati ya Mercy Chinwo na aliyekuwa meneja wake Ezekiel Onyedikachukwu maarufu kama EeZee Tee.

Kwa maoni yake, VDM alihisi kwamba Chinwo hakuwa mkweli na hakutoa maelezo yote kuhusu mzozo kati yake na Eezee Tee, usemi ambao ulimghadhabisha Chinwo.

Mwimbaji huyo aliwasilisha kesi mahakamani ya kuchafuliwa jina na VDM huku akidai fidia ya Naira bilioni 1.1.

Punde baada ya kufahamu kuhusu kesi hiyo, VDM ambaye yuko nchini China alijitetea akisema angependelea wasameheane kwani hawezi kumudu fidia hiyo iwapo atashindwa kwenye kesi hiyo.

Lakini baadaye alionekana kubadili msimamo na amekuwa akiendeleza uchokozi ambapo siku kadhaa zilizopita alisema anataka kurekodi wimbo wa kumtukana Mercy Chinwo na angependa kuhusisha msanii Portable.

Website |  + posts
Share This Article