Mwanamuziki maarufu wa Tanzania, Vanessa Mdee, amezua mazungumzo kuhusu imani, maadili kujitolea kwa baadhi ya watu kwa ajili ya umaarufu, baada ya kufichua ukweli wa kustaajabisha kuhusu sekta ya muziki.
Katika mahojiano na Clouds Digital, nyota huyo wa zamani wa Bongo Flava alielezea sekta ya muziki kama ya kishetani na kishirikina.
Mdee alifunguka kuhusu giza lililofunika kazi yake na hatimaye kusababisha astaafu ghafla mwaka 2020.
Anasema watu wanatumia miungu sana huku akichora picha ya sekta ambayo kwa wengine, makubaliano ya kiroho yanaonekana kuwa bora kuliko kipaji na kazi ngumu.
“Sekta sio ya kupendeza kama inavyoonekana” Mdee alifichua akiongeza kwamba “Nyuma ya pazia kuna giza kubwa—mashirikiano ya kishetani, tabia za kutiliwa shaka, na kupoteza nafsi”.
Alieleza kwamba kuachana na umaarufu kulikuwa ni njia yake ya kurejesha amani na roho yake.
Mdee anasema aligundua anageuka kuwa mtu ambaye hangeweza kumtambua. Shinikizo la kujirekebisha, ulafi, na udanganyifu vikimwathiri.
Moja ya matukio ya kushangaza zaidi katika kazi yake lilitokea mapema, wakati wa mazungumzo na meneja wake. Alikumbuka meneja huyo akimwambia kuwa kabla ya kutoa muziki, ilibidi upelekwe kwa waganga ili kuhakikisha mafanikio.
Alishangazwa na pendekezo hilo akataka kufahamu kuhusu imani ya meneja huyo ambaye alimwambia kwamba naye pia anaamini Mungu lakini huo ni utamaduni.
Mrembo huyo alifichua kwamba baadhi ya timu za usimamizi zinaweka vikwazo waziwazi kwa watu kuhusu kutoa imani yao.
“Kuna timu za usimamizi ambazo zitakuambia waziwazi, kwa kusaini nasi, hautaruhusiwa kutaja jina la Yesu kwenye nyimbo zako,” Vanessa alisema.
Vikwazo hivi vinavuka mipaka ya ubunifu, mara nyingi vikishinikiza wasanii kuingia katika makubaliano ambayo yanaweza kuwa kinyume na imani zao binafsi.
Vanessa alielezea makubaliano kama haya kama ya kiroho ni magumu kukubali na kuacha wasanii wengi wakiwa wanahisi kuzuiwa katika ufanisi wao.
Kwa Vanessa, mvutano kati ya imani na umaarufu ni mapambano ya kimya ambayo wengi katika sekta hiyo wanapitia. Anasema ni rahisi kujikuta kwenye maagano ambayo si ya Mungu.
Akiwa kwenye ndoa na mwigizaji wa Marekani Rotimi, Vanessa anasema uponyaji wake wa kiroho na kihisia unategemea imani yake na familia.
“Nilipata amani kupitia Mungu na familia. Nilijua kuwa kuna zaidi ya maisha kuliko umaarufu, pesa, au nguvu. Maisha hayo hayakuwa yanaridhisha” alielezea.
Hii sio mara ya kwanza kwa Vanessa Mdee kuzungumzia changamoto kubwa alizokutana nazo katika kazi yake ya muziki.
Mwaka 2020, wakati wa mahojiano ya kutangaza kustaafu kwake, alissema sababu ya kuacha muziki ni hitaji la kuchagua maisha yake.