Van Nistelrooy aigura Man Utd

Martin Mwanje
1 Min Read

Kaimu kocha wa timu ya soka ya Uingereza ya Man Utd Ruud van Nistelrooy ameondoka kwenye timu hiyo.

Hii ni baada ya kocha mpya wa mashetani hao wekundu Ruben Amorim kutua Uingereza jana Jumatatu.

Punde baada ya Amorim kuwasili, ilibainika kuwa Van Nistelrooy hakuhitajika katika timu ya wakufunzi wa kocha huyo mpya.

Van Nistelrooy mwenye umri wa miaka 48 alichukua hatamu za kuiongoza Man Utd baada ya kupigwa kalamu kwa Mholanzi Ten Hag.

Mchezaji huyo wa zamani wa Man Utd alijiunga na timu hiyo mwezi Julai mwaka huu kama kocha msaidizi.

Alitia kandarasi ya kumsaidia Ten Hag kunoa makali ya Man Utd kwa kipindi cha miaka miwili.

Kwa kipindi ambacho amekuwa kaimu kocha wa Man Utd, Van Nistelrooy alionekana kupendwa na mashabiki wa timu hiyo na ni wazi kuwa aliandikisha matokeo bora.

Mechi ya mwisho ya Van Nistelrooy ilikuwa dhidi ya Leicester City uwanjani Old Trafford mwishoni mwa wiki iliyopita.

Man Utd ilivuna ushindi mnono wa magoli matatu kwa sifuri wakati wa mechi hiyo na kujizolea alama tatu muhimu.

Ripoti zinaashiria kuwa huenda Van Nistelrooy akateuliwa kuwa kocha wa timu ya AS Roma ya Italia.

Share This Article