Jukwaa la video mitandaoni la Netflix limetangaza kuahirishwa kwa uzinduzi wa kipindi cha Meghan Markle kiitwacho ‘With Love’.
Haya yanajiri wakati ambao mwigizaji huyo wa awali anaangazia kutoa usaidizi kwa waathiriwa wa moto katika eneo la Los Angeles nchini Marekani.
Netflix ilitoa tangazo hilo jana Jumapili ambapo ilitoa taarifa kwenye tovuti yake ikielezea sababu za kuahirisha uzinduzi wa kipindi hicho ‘With Love, Meghan’.
Kulingana na Netflix Meghan ndiye aliomba uzinduzi huo uahirishwe.
Kipindi hicho kimetajwa na wengi kuwa kinachoangazia mapenzi aliyonayo Meghan kwa mvuto wa California Kusini na inaeleweka ni kwa nini hangeweza kukizindua wakati huu eneo hilo linakumbwa na mkasa.
Markle naye alitoa taarifa akishukuru washirika wake Netflix kwa kumuunga mkono na kuahirisha uzinduzi huo ili aangazie mahitaji ya walioathiriwa na moto katika jimbo alilozaliwa la California.”
Meghan na mume wake Prince Harry, walifika katika eneo la mkasa ambapo walionekana wakizuru kujionea athari za moto huo katika makazi ya Pacific Palisades yaliyo magharibi mwa Los Angeles.
Walionekana wenye masikitiko walipokuwa wakizuru eneo hilo huku wakisema na maafisa waliokuwepo.
Moto wa Palisades umechoma eneo la zaidi ya ekari elfu 23 tangu ulipoanza Jumanne na bado unaendelea kuwaka. Kwa jumla eneo la ekari elfu 40 limechomeka huku watu zaidi ya 20 wakiripotiwa kufa moto.
Kipindi hicho cha ‘With Love, Meghan’ kilichokuwa kimepangiwa kuzinduliwa Januari 15, 2025, sasa kitazinduliwa Machi 4, 2025.