Uwezekano wa mvua za El Niño unaongezeka, yaonya Mamlaka ya Hali ya Hewa

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini inasema tukio la El Niño mwaka huu linaendelea kuimarika katika sehemu ya kati hadi mashariki ya Pasifiki ya Ikweta.

KBC Digital News
4 Min Read

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Kenya, KMSA inaonya kuwa kuna uwezakano mkubwa wa nchi hii kukumbwa na mvua za El Nino kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu. 

Kulingana na Mamlaka hiyo, taarifa za hivi karibuni zinaashiria uwezekano wa nchi hii kukumbwa na mvua hizo.

“Tukio la El Niño la mwaka 2026 linaendelea kuimarika katika sehemu ya kati hadi mashariki ya Pasifiki ya Ikweta. Kiashiria cha jadi cha Niño 3.4 kinaonyesha ongezeko la wazi na endelevu, huku wastani wa hivi karibuni wa msimu wa Mei-Julai 2026 ukifikia +1.51°C,” ilisema KMSA kwenye taarifa.

“Tathmini ya mwezi Julai pia iliongezeka hadi +2.03°C. Aidha, kiashiria cha hivi karibuni cha kila wiki cha Niño 3.4, kilichotabiriwa 12 Agosti 2026, kilifikia +2.7°C. Uchunguzi huu unaonyesha kwamba El Niño inaendelea kuimarika zaidi na kuelekea kuwa tukio lenye nguvu zaidi.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika msimu huu, mgao wa mvua katika maeneo mengi nchini unatarajiwa kuwa wa wastani hadi wa kuridhisha, isipokuwa maeneo ya Kaunti za Turkana na Samburu ambapo mgao huu unatarajiwa kuwa wa duni hadi wastani.

Utabiri unaonyesha kuwa mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika kaunti za Baringo, Bomet, Bungoma, Busia, Elgeyo-Marakwet, Embu, Garissa, Homa Bay, Isiolo, Kajiado na Kakamega.

Kaunti zingine ni Kericho, Kiambu, Kilifi, Kirinyaga, Kisii, Kisumu, Kitui, Kwale, Laikipia, Lamu, Machakos, Makueni, Mandera, Meru, Migori, Mombasa, Murang’a, Nairobi, Nakuru, Nandi, Narok, Nyamira, Nyandarua, Nyeri, Siaya na Taita Taveta.

Aidha, kaunti za Tana River, Tharaka-Nithi, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Vihiga, Wajir, pamoja na sehemu kubwa za kaunti za West Pokot, Samburu na Marsabit zitakumbwa na mvua za juu za wastani.

Msimu wa mvua za vuli ambacho ni kipindi cha miezi ya Oktoba–Novemba–Disemba (OND) ni msimu muhimu wa mvua humu nchini hasa katika kaunti za Garissa, Wajir, Mandera, Marsabit, Isiolo, Meru, Tharaka Nithi, Makueni, Kitui, Taita Taveta na Machakos, pamoja na baadhi ya maeneo ya Kajiado na Tana River.

Kwa kipindi hicho, mvua za msimu huo huchangia zaidi ya 40% ya jumla ya mvua katika mwaka. Pia, katika baadhi ya maeneo nchini, zaidi ya milimita 700 za mvua hupokelewa wakati wa msimu huu.

Msimu huu huchochewa na Mzunguko wa Ukanda wa kietropiki, (Intertropical Convergence Zone – ITCZ), ambao hupitia mara mbili nchini, jua likiwa linateremka kutoka Kaskazini kuelekea Kusini (Msimu wa Vuli), na Kusini kuelekea kaskazini (Msimu wa masika).

Muda na utendaji wa msimu huu huathiriwa na Dipole ya Bahari ya Hindi (IOD), ambayo husababisha mvua kuwa zaidi ya kiwango cha kawaida maeneo mengi inchini, inapokuwa katika awamu chanya (positive phase).

Hali ya El Niño, ambayo kwa sasa ni ya kiwango cha juu, pia huelekeza mvua kuwa ya kiwango cha juu zaidi ya kawaida inapoambatana na IOD chanya.

Kwa upande mwingine, msimu wa Oktoba, Novemba na Desemba (OND) nchini Kenya kwa ujumla huwa na hali ya joto, ambapo wastani wa joto huanzia takribani 17°C katika kaunti za Kericho na Uasin Gishu, hadi zaidi ya 30°C (Climatology) katika baadhi ya maeneo ya kaunti ya Turkana.

Hali hii ya joto huchochewa na Mzunguko wa Ukanda wa kietropiki, (Intertropical Convergence Zone – ITCZ), unapotokea Kusini kuelekea Kaskazini au kinyume chake.

Msimu huu wa vuli, joto linatabiriwa kuwa la juu kuliko wastani kwenye maeneo mengi inchini, huku uwezekano mkubwa zaidi ukitarajiwa katika kaunti za Kwale, Mombasa, Kilifi, Lamu, pamoja na baadhi ya maeneo ya Tana River, Taita Taveta na Garissa.

 

 

Share This Article