Sherehe za mwaka huu za siku ya Mashujaa zitaandaliwa katika uwanja wa michezo wa Kericho Green Ijumaa Oktoba 20.
Kamati andalizi ya sherehe za kitaifa ikiongozwa na katibu katika wizara ya mambo ya ndani Dr. Raymond Omollo na Waziri wa Afya Susan Nakhumicha imezuru uwanja huo leo kuhakikisha uko tayari kwa hafla hiyo.
Akizungumza na wanahabari baada ya ukaguzi huo, Waziri Nakhumicha aliridhika na maandalizi ya kamati hiyo huku akikaribisha wakenya wote, hasa wakazi wa kaunti ya Kericho, kuhudhuria sherehe hizo.
Ikitizamiwa kwamba mandhari ya sherehe za mwaka huu ni kuendeleza mpango wa huduma bora za afya kwa wote, waziri huyo amekita kambi katika kaunti ya Kericho ambapo jana aliongoza Naibu Rais Rigathi Gachagua katika kuzuru miradi kadhaa ya sekta ya afya kwa nia ya kujifahamisha.
Katibu Omollo kwa upande wake alielezea kwamba wameshuhudia mazoezi ya wahusika kadhaa wa sherehe za Ijumaa zitakazoongozwa na Rais William Ruto wakiwemo wanajeshi na wasanii na kwamba ana uhakika wako tayari.
Aliongeza kwamba wamechagua mashujaa wapatao 250 ambao wataenziwa siku hiyo na kwamba kwa wiki nzima watakuwa wanaonyesha mambo kadhaa ambayo serikali imetekeleza katika sekta ya afya kwa lengo la kuboresha huduma.