Uwanja wa JKIA umeuzwa? Huo ni uongo, asema Mudavadi

Martin Mwanje
2 Min Read

Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi amekanusha madai kwamba Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA umeuzwa. 

Madai yamechipuka katika siku za hivi karibuni kwamba uwanja huo umeuzwa, na Seneta wa kaunti ya Kisii Richard Onyonka ni miongoni mwa walionukuliwa wakisema kuna mipango ya kuuza uwanja huo.

“Wacha nifutilie mbali mara moja madai kuwa Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA unataka kuuzwa. Hii ni mali ya umma, ni mali ya kimkakati, na ikiwa kungekuwa na mipango ya kuiuza, unaweza tu ukafanya hivyo baada ya mchakato kamili wa umma ambao umeidhinishwa na bunge,” alisema Mudavadi alipofika mbele ya bunge jana Jumatatu.

“Kwa hivyo, yeyote anayetoa dhana kwamba uwanja wa JKIA umeuzwa hasemi ukweli, si ukweli.”

Mudavadi ambaye pia ni kinara wa mawaziri badala yake ameelezea haja ya kuufanya uwanja wa JKIA kuwa wa kisasa kwa kujenga vituo vingine vya abiria.

Ametoa wito kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini, KAA kuangalia kwa makini mipango yake ya uwekezaji na kuhakikisha kila kitu kinaendeshwa kwa uwazi ili kuzuia visiki vya kisheria wakati wa mchakato wa upanuaji.

Mpango wa kujenga kituo cha abiria cha Greenfield Terminal awali ulikumbana na changamoto za kisheria kiasi kwamba mpango huo bado umekwama hadi leo.

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *