Rais William Ruto amemsuta mkandarasi anayekarabati Uwanja wa Michezo wa Bukhungu akimtuhumu kwa kuzembea kazini.
Ingawa ukarabati huo unapaswa kumalizika kufikia katikati ya mwaka 2026, kuna rundo la kazi nyingi ambayo bado haijafanywa.
“Kasi inayotumiwa kukarabati Uwanja wa Bukhungu haikubaliki. Ukarabati huo sharti umalizike katikati ya mwaka 2026,” alisema Rais Ruto alipotembelea uwanja huo jana Jumatano na kukagua kazi inayoendelea ya ukarabati.
Ruto, aliyekuwa ameandamana na Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa na Seneta Boni Khalwale miongoni mwa viongozi wengine, ameiagiza Wizara ya Michezo kupitia upya hatua iliyopigwa katika ukarabati wa uwanja huo ili kuhakikisha unakamilishwa kwa wakati.
Uwanja wa Bukuhungu una uwezo wa kuwatoshea mashabiki 30,000.
Ukarabati wa uwanja huo ulianza wakati wa utawala wa aliyekuwa Gavana wa kaunti ya Kakamega Wycliffe Oparanya.