Uuzaji wa JKIA: KAA yakanusha madai

Martin Mwanje
2 Min Read

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini, KAA hatimaye imesitisha kimya chake na kuzungumia madai kuwa Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA umeuzwa. 

Katika taarifa leo Jumatano, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KAA Henry Ogoye badala yake amebainisha kuwa mamlaka hiyo ilipokea pendekezo la uwekezaji kutoka kwa kampuni ya Adani Airport Holdings Limited ambayo ni mwendeshaji mkuu wa viwanja vya ndege.

Pendekezo hilo lilipokelewa na KAA chini ya Sheria ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Kibinafsi ya mwaka 2021.

Kulingana na Ogoye, pendekezo hilo lilihusu ujenzi wa jengo la kituo kipya cha abiria, barabara ya pili ya ndege na kukarabatiwa wa miundombinu iliyopo kwa sasa iliyochakaa ya JKIA na ambayo mamlaka hiyo imeitaja kuwa tishio kwa ushindani wa kikanda wa JKIA.

“Pendekezo hilo litafanyiwa mapitio ya kiufundi, kifedha na kisheria sambamba na michakato inayohitajika kwa mujibu wa Sheria ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Kibinafsi ya Mwaka 2021,” alisema Ogoye katika taarifa.

“Makubaliano ya mradi huo yatatanguliwa na kuwashirikisha washikadau, na kutafuta idhini kutoka kwa Wizara ya Fedha, Mwanasheria Mkuu na Baraza la Mawaziri.”

Ogoye ametoa hakikisho kuwa hakuna mfanyakazi wao hata mmoja atakayepoteza kazi kutokana na kutekelezwa kwa pendekezo hilo, na kwamba isitoshe upanuzi wa JKIA utabuni fursa zaidi za kibiashara na kuleta faida nyingi.

Jana Jumanne, Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi alikanusha madai kuwa uwanja wa JKIA umeuzwa.

 

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *