Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki ameomba msamaha kutokana na mapungufu ya muda mrefu na ukawiaji unaoshuhudiwa katika utayarishaji wa utoaji wa pasipoti nchini.
Miezi iliyopita, Prof. Kindiki alizuru jumba la Nyayo mara kadhaa akiapa kuwafurusha matapeli wanaotatiza utoaji wa pasipoti kwa wanaozihitaji.
Licha ya ziara hizo, foleni ndefu za watu bado zinashuhudiwa katika jumba la Nyayo huku Wakenya wakihangaika kutafuta stakabadhi hiyo muhimu ya usafiri.
Hali ambayo imemlazimu Prof. Kindiki kuomba msamaha katika kile kinachoonekana kuwa ishara kwamba mageuzi aliyoanzisha katika idara ya uhamiaji ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa baadhi ya maafisa katika idara hiyo hayajazaa matunda yaliyokusudiwa.
“Nawajibika kikamilifu kutokana na ufisadi wa kimfumo ambao umekithiri katika idara ya uhamiaji. Nitafanya kila niwezalo kuwatokomeza matapeli ambao wamekuwa wakivuruga ajenda ya mageuzi yanayokusudia kulainisha michakato ya kupata stakabadhi za usafiri na uraia,” alisema Profl Kindiki.
Kulingana naye, msako mkali umeanzishwa kuwafurusha maafisa ambao bado wanaendelea kujihusisha katika visa vya ufisadi akionya kwamba yeyote atakayepatikana akijihusisha katika uovu huo atakamatwa na kushtakiwa bila kujali hadhi yake.