Uteuzi wa Samuel Maina kama kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KBC watenguliwa

Martin Mwanje
2 Min Read

Samuel Maina kuanzia leo Jumanne, Disemba 19, 2023 siyo tena kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Nchini Kenya, KBC. 

Badala yake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Eliud Owalo amemteua Paul Macharia kuwa kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KBC kuanzia leo Jumanne.

Macharia atakaimu wadhifa huo kwa kipindi cha miezi 6 hadi mchakato wa kumteua Mkurugenzi Mkuu mpya wa KBC unaoendelea utakapokamilika.

Waziri Owalo ameiagiza Bodi ya KBC kuharakisha mchakato huo.

“Kufuatia barua (Mint: KC/MD/5/42//c) iliyoandikwa Disemba 18, 2023 na ambayo kupitia kwake kaimu Mkurugenzi Mkuu ameahidi kwamba Serikali ya Kenya italipa dola bilioni 5 za Marekani katika Korti ya Kimataifa ya Upatanishi ya London, LCIA Namba. 122233: Channel 2 Group Corporation Versus Kenya Broadcasting Corporation bila kutafuta kibali cha Wizara, Hazina Kuu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Idara ya Haki kwa kukiuka kabisa maelekezo ya awali yaliyotolewa kwa shirika la KBC kuhusu suala hilo, naagiza kama ifuatavyo – 1. Uteuzi wa Bw. Samuel Maina kama kaimu Mkurugenzi Mkuu unatenguliwa mara moja 2. Bw. Samuel Maina anapaswa kukoma kuhudumu katika wadhifa huo mara moja na hatua za kinidhamu kuanzishwa dhidi yake na Bodi…,” ameagiza Waziri Owalo katika taarifa.

Maina aliteuliwa kuwa kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la KBC baada ya kipindi cha kuhudumu cha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Naim Bilal kumalizika.

Kabla ya kuteuliwa kuwa kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KBC, Maina alihudumu kama Mhariri Mkuu wa shirika hilo.

Hadi kuteuliwa kwake kama kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KBC, Macharia amekuwa akihudumu kama mtaalam wa Uchumi wa Mawasiliano katika Sekretariati ya Kitaifa ya Mawasiliano iliyo chini ya mamlaka ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali.

Share This Article