Uteuzi wa Dorcas Oduor, Beatrice Askul waidhinishwa na bunge

Martin Mwanje
1 Min Read
Dorcas Oduor aliyeteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu

Bunge la Kitaifa limeidhinisha uteuzi wa Dorcas Oduor kuwa Mwanasheria Mkuu na Beatrice Askul Moe kuwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda. 

Oduor sasa anatarajiwa kujaza pengo lililoachwa wazi na Justin Muturi aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma huku Askul akimrithi Peninah Malonza katika Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda.

Wawili hao sasa wanasubiri kuteuliwa rasmi na Rais William Ruto.

Oduor anatarajiwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kuhudumu kama Mwanasheria Mkuu humu nchini ikiwa atateuliwa rasmi katika wadhifa huo.

Wakati akisailiwa na kamati ya bunge juu ya uteuzi, Oduor alisema ikiwa uteuzi wake utaidhinishwa, utakuwa wajibu wake kuzitathmini kwa makini kesi kabla ya kuziwasilisha mahakamani.

Aliyasema hayo wakati ambapo serikali imekuwa na hulka ya kupoteza kesi nyingi zilizowasilishwa mahakamani.

Oduor amesema hatua hiyo itasaidia kuepusha serikali kukumbwa na hasara kubwa zinazotokana na kupoteza kesi zinazowasiliswa mahakamani.

“Itakuwa pia kazi yangu kuzishauri wizara, idara na mashirika kuhusu namna ya kushughulikia kesi mahakama,” alisema Oduor Ijumaa wiki iliyopita wakati akisailiwa na kamati ya bunge kuhusu uteuzi iliyoongozwa na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula.

 

 

Share This Article