Wabunge wanaogemea mrengo wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa wanashinikiza kubuniwa kwa tume huru ya umma ya uchunguzi ili kuchunguza ongezeko la visa vya utekaji nyara vinavyoshuhudiwa nchini.
Wakiwahutubia wanahabari katika majengo ya bunge leo Jumanne, wabunge hao pia wanatoa wito kwa serikali ya Kenya Kwanza kuhakikisha watu waliosalia waliotekwa nyara wanaachiliwa huru.
Kwenye taarifa iliyotiwa saini na Wabunge na Maseneta wapatao 25, wote hao pia wanaitaka tume hiyo kukabidhiwa jukumu la kuchunguza kuingizwa kwa siasa kwenye idara ya polisi na taasisi zingine huru.
Kulingana nao, tume hiyo pia inapaswa kuchunguza mashambulizi yaliyopangwa dhidi ya Gachagua ikiwa ni pamoja na vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa mazishi huko Limuru.
Aidha, wanataka kuibuka tena kwa magenge ya uhalifu ikiwa ni pamoja na Mungiki kufanyiwa uchunguzi.
“Tunatoa wito kwa Bunge la Taifa, Seneti na pia Mabunge yote ya Kaunti kote nchini kuandaa vikao maalum wakati wa mapumziko kujadili na kufanya uchunguzi juu ya visa hivi vya utekaji nyara na masuala mengine muhimu yanayoathiri jamii yetu,” walisema wabunge hao kwenye taarifa.
Miongoni mwa wabunge waliotia saini taarifa hiyo ni Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang’wa na wabunge John Kaguchia (Mukurweini), Onesmus Ngogoyo (Kajiado Kaskazini), Wanjiku Muhia (Kipipiri) na Gathoni Wamuchomba (Githunguri) miongoni mwa wengine.
Pendekezo lao linajiri siku moja baada ya baadhi ya vijana waliotekwa nyara kuachiliwa huru jana Jumatatu.
Polisi wamekana kuhusika katika utekaji huo na wanasema watawahoji vijana hao kwa lengo la kupata taarifa inayohusiana na utekaji nyara wao.
Taasisi na viongozi mbalimbali wamelaani vikali visa vya utekaji nyara nchini na kutaka jinamizi hilo kukomeshwa mara moja.