Utafiti umebaini kwamba kuna pengo katika sekta ya benki nchini kutokana na ukosefu wa maoni ya wataalam kuhusu utendaji kazi katika sekta ya benki.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya hivi punde iliyoandaliwa na kampuni ya utafiti barani Afrika, Agusto.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Yinka Adelekan anasema tafiti kadhaa zimefanywa na ripoti kutolewa kuhusu sekta ya benki nchini zikiwemo ripoti za Benki Kuu ya Kenya na chama cha wadau wa benki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mwaka huu kuhusu sekta ya benki, Adelekan alisema licha ya changamoto hizo, kampuni yake ilipata fursa ya kutathmini hali ya sekta ya benki nchini na kukadiria uwezo wake wa kutoa mikopo na jukumu la kuinua uchumi wa taifa.
Mtaji wa taasisi za kifedha nchini kwa mujibu wa ripoti hiyo ni Benki ya Kenya Commercial, KCB asilimia 14.7, Benki ya Equity asilimia 13.5, Benki ya Cooperative asilimia 9.40, Benki ya NCBA asilimia 8.53 na Benki ya Absa asilimia 7.24.