Ustaarabu wa kale wa China unaendelea kuchochea maendeleo ya taifa hilo

Tom Mathinji
10 Min Read

China Media Group (CMG) hivi karibuni ilitoa mfululizo wa kipindi cha televisheni kwa jina “Classics of Chinese Thought”. Kipindi hicho kinaangazia mazungumzo na mahojiano yanayowajumuisha wasomi na wataalam kuhusu ufamahu wa historia ya ustaarabu wa China.

Aidha, kipindi hicho kinaelezea umuhimu wa mwendelezo wa utamaduni wa jadi wa China, pamoja na jinsi mwendelezo wa ustaarabu huu umechangia maendeleo ya jamii ya China. Wale walioangaziwa haswa wanazungumzia jinsi njia hii ya kipekee ya maisha imekuwa msingi wa maendeleo ya kasi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni.

Ustaarabu wa Kichina unatambuliwa sana kama moja ya ustaarabu wa zamani zaidi unaoendelea na ambao pia umedumisha mila, falsafa, sanaa, fasihi, na sayansi.

Kipindi hiki cha CMG kinatambulisha ulimwengu kwa sifa tano maarufu za utamaduni huo zikiwemo mwendelezo, ubunifu, umoja, amani na ya ushirikishwaji, na ambazo kwa pamoja  zinachangia maadili na mifumo yake ya kina.

Kutoka masuala hayo matano, mada inayodhihirika ni ile ya taifa na watu wenye hamu ya kudumisha utambulisho tofauti na kuinuka pamoja na wengine, bila ya kutaka kufaida pekee.

Kuelewa ustaarabu huu, kwa hivyo, ni hatua ya kwanza kabisa katika kuelewa China. Rais Xi Jinping mara kwa mara amesema kuwa haiwezekani kuielewa China, ya zamani na ya sasa, ikiwa mtu hataielewa China kupitia mwendelezo wa historia yake ndefu.

Baadhi wamehoji kuwa maendeleo ya kasi ya China  yametokana na mwendelezo wake wa kitamaduni usioingiliwa, na ni rahisi kuona ni kwa nini. Mwendelezo huu kwa muda, kama ilivyoonyeshwa katika kipindi hicho, imechangia ukusanyaji wa maarifa na hekima, na kusababisha mageuzi nchini China na kufanya jamii ya Wachina kuwa jinsi walivyo kwa sasa.

Kwa kuukumbatia urithi wake wa kitamaduni, Rais Xi anasema China imeweza “kudumisha uhusiano wa kina na mizizi yake, na kukuza hisia ya utambulisho wa kitamaduni pamoja na kupiga hatua kubwa ya kusonga mbele.”

Mwendelezo

Falsafa ya Confucius imechangia pakubwa katika uendelezaji wa ustaarabu wa Kichina. Falsafa hii ni wazo lililoanzishwa na mwanafalsafa wa kale wa Kichina, na mwalimu maarufu kwa jina Confucius. Tunajifunza kwamba mawazo yake yalilenga kujenga jamii yenye usawa na ya haki kupitia ukuzaji wa maadili, mwenendo, na maelewano ya kijamii.

Falsafa ya Confucius imekuwa na ushawishi mkubwa takriban kakika kila nyanja ya jamii ya Kichina, ikiwa ni pamoja na utamaduni, elimu, na siasa.

Profesa Kong Xinfeng wa Chuo Kikuu cha Minzu cha China katika mkoa wa Shandong, unaochukuliwa kuwa mahali pa kuzaliwa kwa utamaduni wa Confucius, anasema Confucius alitekeleza wajibu mkubwa wa kupitisha ustaarabu wa China. Anasema Confucius ni mwalimu mkuu wa watu wa China.

“Leo hii, mawazo yetu na tabia zetu, zimeshawishiwa mno na mafunzo ya Confucius,” alisema

Anataja mafundisho kama vile vya “kutawala kwa wema na daima kutafuta kujiboresha bila kukoma” kama mafundisho yaliyo na ushawishi mkubwa kwa Wachina. Anaamini kuwa mwendelezo wa ustaarabu wa China umeisaidia taifa hilo lililo Asia Mashariki kubuni njia mpya ya maendeleo badala ya kuiga kutoka nchi nyingine.

“Usiwatendee wengine kile ambacho hutaki wengine wakutendee.” Profesa Kong anasema ndilo funzo kuu kutoka Confucius inayotoa mwelekeo kwa Wachina wote.

Umoja

Umoja ni nguzo ambayo watu wote wa China wanategemea kwa ustawi wa taifa hilo. Mwanasayansi maarufu wa kisiasa Profesa Zhang Weiwei anasema China imewekeza umuhimu mkubwa kwa masuala ya umoja na anashikilia mtazamo kwamba ustaarabu wa China haujaendelea tu bila kuingiliwa ila pia imedumisha kiwango cha juu cha umoja.

Licha ya ukubwa wake wa kijiografia, makabila mbalimbali, na maendeleo magumu ya kihistoria, China imedumisha umoja na mshikamano.

Nchini China, makabila tofauti yanaendelea kuishi kwa pamoja na kwa amani. Makundi madogo kama vile Zhuang, Hui, Manchu, Uighur, Tibetan, na mengineyo, yameingizwa katika utamaduni wa kabila la Han, na kuchangia umoja wa kitamaduni wa ustaarabu wa China.

Ujumuishaji

Xiang Shuchen ambaye ni msomi katika taasisi ya China National Archives of Publications and Culture anatoa hoja muhimu mno. “Lazima kuwe na utofauti wa vitu ili kustawi na kukua, kwani kukiwa na ufafanaji mambo hayawezi kuwa endelevu,” anasema huku akielezea asili ya umoja wa ustaarabu wa Kichina

Anaendelea kusema: “Rangi moja haiwezi kuwa nzuri kutazama, ladha haina moja haiwezi kuwa ladha nzuri, na kitu kimoja hakiwezi kutathminiwa vilivyo,”

“Kwa zaidi ya miaka 1,000 ya njia ya Silk, vitu vingi tofauti vilibadilishwa. Kando na bidhaa, tamaduni na imani tofauti zilibadilishwa, yote yakiwezeshwa na mazingira ya umoja nchini China,” alieleza

Katika historia yake ndefu, ustaarabu wa China, kwa hivyo, umeonyesha uwezo wa ajabu wa umoja, ukijumuisha makabila mbalimbali, lugha, dini, na mila tofauti ndani ya mfumo wake wa kitamaduni na kisiasa.

Ustaarabu wa Kichina pia una historia ndefu ya wingi wa dini na kuvumiliana, unaojumuisha mila mbalimbali za kidini kama vile Ubuddha, Daoism, Confucianism, Ukristo, Uislamu, na dini za watu wa asili. Mila hizi za kidini zimeishi na kuingiliana, na mara nyingi zinashawishi na kuimarisha imani na mazoea ya kila mmoja.

Utulivu

Historia ya China ya utetezi wa amani inajulikana. Profesa Bai Tongdong kutoka Chuo Kikuu cha Fudan anasisitiza nafasi ya China katika kutoa msukumo kwa  ulimwengu kuthamini amani, huku akisisitiza kuwa maelewano, utulivu, na kutokiuka sheria yanatambulisha China.

Kwa kweli Rais Xi Jinping, mara kwa mara, ameielezea China kama “mjenzi wa amani ya dunia, mchangiaji wa maendeleo ya kimataifa na mtetezi wa utaratibu wa kimataifa”.  Amani hii inaonekana kwa kuwa China inapinga kuingiliwa kwa mambo ya ndani ya nchi nyingine au kuweka maadili yake na mfumo wake wa kisiasa kwa wengine, na badala yake kushinikiza ushirikiano.

Bai Tongdong, ambaye ni mtaalam katika falsafa ya jadi ya kisiasa ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Fudan anasema mafundisho ya Confucius yanasisitiza umuhimu wa tabia ya kimaadili, utaratibu wa kijamii, na kuheshimiana, kukuza uhusiano wa usawa na utatuzi wa migogoro kupitia mazungumzo badala ya nguvu, na hii imejikita sana nchini China.

“Tunahitaji kufanya kitu kizuri kwa ajili ya binadamu wote. Hatufai kuwa na vita, au njaa kubwa, au mauaji ya kimbari, hiyo ni wajibu wa binadamu,” anasema.

Ubunifu

Mfululizo huu wa vipindi pia unazungumzia kichocheo cha uvumbuzi unaoshuhudiwa kwa sasa nchini China, haswa jijini Guangzhou, inayochukuliwa kuwa mji wa uvumbuzi.

Ustaarabu wa China una historia ndefu ya uvumbuzi na maendeleo ya kiteknolojia, na mambo mengi ambayo yamechangia maendeleo ulimwenguni. Ujuzi wa Wachina umesababisha uvumbuzi wa historia katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na teknolojia, sayansi, kilimo, tiba, na uhandisi.

Bwana Yu Pun Hoi kutoka Chuo Kikuu cha Peking anasema Wachina daima huthamini umuhimu wa uvumbuzi na mabadiliko. Ananukuu mashairi ya kawaida kutoka kwa enzi ya Tang yanayosisitiza “uboreshaji endelevu na upya.”

Kuboresha uvumbuzi wa China na ushindani kwa ukuaji wa haraka kunatokana na uwekezaji mkubwa katika sayansi, teknolojia, na uvumbuzi unaoongeza hadhi yake kama taifa lenye ushawishi mkubwa wa kiuchumi duniani.

Ndege kubwa ya abiria ya China maarufu kama C919 imezinduliwa na kuanzisha safari yake ya kibiashara ya kwanza kutoka Shanghai hadi Beijing mnamo Mei 2023.  Ndege hiyo imepata umakini mkubwa ulimwenguni, na inatarajiwa kuwa chombo cha usafiri wa anga mbadala kando na Airbus na Boeing katika soko la ndege za abiria. Mbali na ndege ya C919, China imesifika kwa ujenzi wa meli kubwa za kusafirisha abiria na mizigo, utengenezaji wa magari ya nishati mpya, na kufanya misheni katika anga za juu, kati ya mambo mengine mengi.

Kwa hivyo, ustaarabu wa China, juhudi za maendeleo ya kisasa za nchi pamoja na hatua za ufufuzi zinaunganishwa pamoja. Rais Xi Jinping amesisitiza umuhimu wa urithi na heshima kwa utofauti wa ustaarabu huu, na kutetea mpango wa ustaarabu wa kimataifa.

Mpango huu, GCI, una lengo la kukuza heshima kwa mila tofauti, maadili ya msingi ya ubinadamu, umuhimu wa urithi na uvumbuzi wa ustaarabu, pamoja na ushirikiano na ubadilishanaji wa mawazo baina ya watu kutoka mataifa mbalimbali. Mpango huo unapendekeza njia ya kujenga taifa lenye nguvu la China, na kuchangia maendeleo ya ubinadamu na maelewano kwa ulimwengu wote.

Eric Biegon ni mwandishi wa habari katika Shirika la Utangazaji la Kenya, KBC.

Share This Article