Usher asema amesubiri maisha yake yote kutumbuiza kwenye Super Bowl

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Marekani Usher Raymond IV maarufu kwa jina lake moja Usher amesema kwamba amekuwa akisubiri maisha yake yote kutumbuiza kwenye tamasha fupi ya katikati ya mechi ya soka ya Super Bowl nchini Marekani ambayo inafahamika kama, “Super Bowl Halftime Show”.

Kulingana naye, dakika 13 za tamasha hiyo fupi ni muhimu sana kwani kila msanii huenzi kutumbuiza katika jukwaa hilo ambalo wengi wameweza kutumbuiza.

Akizungumza kwenye mahojiano katika runinga ya CBS, Usher wa umri wa miaka 44 sasa, alisema kwamba miaka 30 iliyopita alijitolea kuhakikisha ubora katika kazi yake kama mwanamuziki na sasa kujitolea kwake kunazawadiwa na fursa hii ya kipekee ya Super Bowl.

Mwimbaji huyo ameahidi mashabiki tamasha bora siku hiyo, akisema itakuwa sherehe.

Usher anasema alifahamu mapema kuhusu kuhusishwa kwenye Super Bowl awamu ya 58 itakayoandaliwa Februari 11, 2024, lakini hakuamini alipopatiwa mwaliko rasmi na Jay Z ambaye ni mmoja wa watayarishaji wa tamasha hiyo.

Jay Z alimwambia, “Ni wakati wako. Wakati wa kipekee”.

Watoto wa Usher pia wamekuwa wakitaka atumbuize kwenye tamasha hiyo, huku mashabiki wakianzisha ombi kwenye mitandao ya kijamii.

Wanamuziki wengi wametunukiwa fursa ya kutumbuiza kwenye Super Bowl wakiwemo Michael Jackson, Beyoncé na Prince, na Usher anasema ari yake ni kuhakikisha tumbuizo lake linaafiki viwango vilivyowekwa na watangulizi wake.

Awamu ya 58 ya Super Bowl itaandaliwa katika uwanja wa Allegiant huko Las Vegas Februari 11 mwakani na mchuano mzima wa soka pamoja na tamasha ya dakika 13 wakati wa mapumziko vitapeperushwa moja kwa moja kwenye runinga ya CBS.

Share This Article