Ushauri wa Akothee kwa Simon na Sarah Kabu

Unajiri baada ya wanandoa hao kutangaza utengano wao kufuatia kufujishwa kwa video ya kamera ya siri ya nyumbani kwao. sarah Kabu anaonekana kwenye video hiyo akimpiga mwanamke fulani.

Marion Bosire
2 Min Read

Simon na Sarah Kabu wanandoa maarufu mitandaoni na wamiliki wa kampuni ya Bonfire Adventures waliashiria kwamba wametengana kupitia mitandao ya kijamii.

Hatua hiyo ilijiri baada ya video ya kamera fiche ya nyumbani kwao kusambazwa mitandaoni ikimwonyesha Sarah akimzaba makofi binti ambaye anasemekana kuwa kijakazi huku wengine wakisema ni mpenzi wa Simon.

Mwanamuziki Akothee sasa anashauri wawili hao kujiondoa kwa muda kutoka kwenye mitandao ya kijamii ili wasuluhishe tofauti zao.

Kulingana naye, wafuasi wa mitandaoni hawatawasaidia kwani ushahidi wanaoomba kutoka kwao utatumika tu kuwadhalilisha zaidi.

“Kinachoendelea sio kizuri kwenu na kwa wanafamilia wenu hasa watoto wenu.” aliandika Akothee akiendelea kusema kwamba watu wanaoeleza kilichotokea mitandaoni wanajumuisha waliopitia magumu kwenye ndoa.

Anawashauri wasiendelee kujaribu kuharibiana sifa akisisitiza kwamba ushahidi wanaotoa mitandaoni utawaumiza siku zijazo.

“Ninasisitiza. Kabu nyamaza. Wewe ni mwanaume, baba na mfanyabiashara. Toka kwa kamera kwanza. Suala hili ni nyeti mno kuanikwa mtandaoni kwa sasa.” alishauri Akothee.

Aliendelea kwa kukiri kwamba aliwahi pitia tukio sawia ambapo aliyekuwa mume wake aliharibu ndoa yao na kisha kushawishi kila mmoja kwamba yeye ndiye alikuwa tatizo.

Kwa mara ya kwanza amefichua kwamba mwanamke aliyechukua mahala pake naye alimwacha mume wake wa zamani.

“Kilicho mahakamani acha kiendelee.Hawa watu wa mitandao ya kijamii sio watu wazuri.” alimalizia Akothee.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *