Urusi yaonya ECOWAS dhidi ya kutuma wanajeshi Niger

Tom Mathinji
1 Min Read

Urusi imeionya Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi Ecowas, kuhusu kuchukua hatua za kijeshi ambazo inasema itachukua dhidi ya wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Niger.

Inasema kuwa uamuzi huo unaweza kusababisha mgogoro ambao hautaonekana kwa muda mrefu.

Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia siku ya Ijumaa, ilizionya nchi za Afrika Magharibi kutopeleka wanajeshi Niger.

Taarifa hiyo ilisema, “Tunaamini kwamba hatua hiyo ya kijeshi haitatatua tatizo la Niger, badala yake hali hiyo itasababisha mzozo mkubwa, ambao tarehe yake haijulikani, na hali katika eneo la Sahel itakuwa ngumu tena”.

Wakuu wa usalama wa Ecowas wanapanga mkutano siku ya Jumamosi kupanga jinsi ya kuandaa jeshi.

Siku ya Ijumaa, kundi la Ecowas lilikubali kuanzisha ‘kikosi cha kudumu’ katika maandalizi ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya jeshi la Niger.

Tayari, rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, alisema kuwa nchi yake itatuma takriban wanajeshi 1,000 ambao watajiunga na safu ya vikosi vingine vya kijeshi ambavyo vitakuwa kwenye mpango wa kutumwa Niger.

Marekani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya tayari zimeunga mkono uamuzi uliochukuliwa na kundi la Ecowas kumrejesha madarakani rais mteule Mohamed Bazoum.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *