Urusi yaamuru watu kuhamishwa baada ya shambulio la Ukraine la ndege zisizo na rubani

Martin Mwanje
1 Min Read

Wakazi katika baadhi ya sehemu za eneo la Tver nchini Urusi wameamriwa kuhama baada ya shambulio “kubwa” la Ukraine ya ndege zisizo na rubani kuzua moto, gavana wa eneo hilo amesema.

Igor Rudenya alisema wafanyakazi wa huduma za dharura katika mji wa Toropets wamekuwa wakijaribu “kuzima” moto uliosababishwa na kuanguka kwa mabaki ya ndege zisizo na rubani. Hakusema iwapo kuna majeruhi.

Wakati huo huo, picha ambazo hazijathibitishwa zimeibuka zikionyesha mlipuko mkubwa katika mji huo.

Kanda za video zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha milipuko na moshi mkubwa ukitanda angani.

Mashirika ya habari ya AFP na Reuters yamenukuu vyanzo vya Ukraine vikisema ghala la risasi lilipishambuliwa.

Mkuu wa Kituo cha Ukraine cha Kukabiliana na taarifa za upotoshaji Andriy Kovalenko, alisema kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba pamoja na silaha zake kama vile roketi za Grad na makombora mbalimbali, Urusi pia imeanza kuhifadhi makombora ya Korea Kaskazini katika eneo la Toropets.

BBC haijathibitisha madai yoyote yaliyotolewa.

Toropets iko karibu kilomita 380 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Urusi Moscow, na kilomita 470 kaskazini mwa mpaka na Ukraine.

Share This Article