Siku tatu baada ya shambulio la kuvuka mpaka la Ukraine katika eneo la Kursk nchini Urusi, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Moscow lazima “ihisi” matokeo ya uvamizi wake Ukraine.
“Urusi ilileta vita katika ardhi yetu na inapaswa kuhisi kile ilichokifanya”, Bw Zelensky alisema katika hotuba yake ya Alhamisi jioni, bila kuyazungumzia moja kwa moja mashambulizi ya Ukraine.
“Waukreni wanajua jinsi ya kufikia malengo yao. Na hatukuchagua kufikia malengo yetu katika vita,” aliongeza.
Urusi inasema takriban wanajeshi 1,000 wa Ukraine, wakisaidiwa na vifaru na magari ya kivita, waliingia katika eneo lake Jumanne asubuhi – katika kile kinachoonekana kuwa moja ya mashambulio makubwa zaidi katika ardhi ya Urusi tangu vita kuanza.
Rais wa Urusi Vladimir Putin hapo awali aliishutumu Ukraine kwa “chokozi kubwa”.
Maafisa wa Ukraine wamekuwa kimya kwa kiasi kikubwa kuhusu mashambulizi hayo. Ni vigumu kuelewa hali halisi katika uwanja wa vita na ni maelezomachache yametolewa kutoka kila upande.