Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya umeitaka huduma ya taifa ya polisi kutovuruga maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha 2024 yanayotarajiwa kuandaliwa leo Jumanne.
Kupitia kwa taarifa Jumatatu jioni, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka aliwalaumu maafisa wa polisi kwa kuvuruga maandamano ambayo huwa ya amani.
“Tunawaagiza maafisa wa polisi kukoma kuwatisha, kuwaogofya na kuwadhulumu Wakenya wanaoshiriki maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha 2024,” alisema Kalonzo.
Taarifa hiyo ya Azimio ilijiri muda mfupi baada ya Waziri wa Usalama wa Taifa Prof. Kithure Kindiki kuwaagiza waandamanaji kuzingatia sheria wanaposhiriki maandamano.
Hata hivyo, Azimio imeonya kuwa afisa yeyote wa polisi atakayevuruga maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha 2024 atawajibikia hatua yake.
Vijana hapa nchini kwa jina Gen Z wamekuwa wakishiriki maandamano kote nchini ili kuwashinikiza wabunge kupinga mswada huo ambao wameutaja kandamizi na unaowaongezea mzigo mkubwa.