Upinzani uliojihami nchini Syria umesema kwamba umechukua udhibiti wa jiji kuu Damascus na kwamba Rais Bashar al-Assad ametoroka kutoka nchi hiyo.
Kamanda wa kundi la waasi la Hayat Tahrir al-Sham Abu Mohamed al-Julani amesema kwamba asasi zote za serikali zitasalia chini ya usimamizi wa waziri mkuu wa Assad hadi zitakapokabidhiwa kwao rasmi.
Tangazo lake linajiri saa chache baada ya makundi ya upinzani kuteka miji kadhaa nchini Syria.
Mataifa ya Qatar, Saudi Arabia, Jordan, Egypt, Iraq, Iran, Turkiye na Russia yametoa taarifa ya pamoja yakionya kwamba yanayoendelea nchini Syria ni hatari na kupendekeza suluhisho la kisiasa.
Waziri mkuu wa Syria Mohammed al-Jalali amesema kwamba yuko tayari kuunga mkono mpito wa mamlaka na kushirikiana na upinzani.
Waasi wa upinzani nchini Syria walitangaza kupitia runinga inayomilikiwa na serikali kwamba utawala wa Bashar al-Assad umepinduliwa.
Walipoingia jijini Damascus, waasi hao walifungulia wafungwa waliokuwa gerezani huku Rais Assad akitoroka.