Pilikapilika za upanzi wa miti zilipamba moto humu nchini huku Rais William Ruto akizindua siku ya kitaifa ya upanzi wa miti katika eneo chepechepe la Kiu, kaunti ya Makueni.
Rais Ruto anasema rasilimali asilia hasa misitu hutekeleza jukumu muhimu katika kudumisha uwiano wa mfumo ikolojia, kuongeza uhai anuwai na kuhakikisha kipato cha watu na jamii kote nchini.
“Utunzaji wa mazingira ni suala la dharura na wajibu wa pamoja wa wakati wetu,” aliongeza Ruto.
Akiandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa nchi aliwahimiza Wakenya kuwa katika mstari wa mbele katika upanzi wa miti katika wito ulioungwa mkono na viongozi waliokuwapo.
Katika maeneo mengine ya nchi, viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri na makatibu wa wizara mbalimbali waliwaongoza Wakenya katika upanzi wa miti wakati huu wa msimu wa mvua.
Serikali inalenga kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka wa 2032.
Ilitenga Novemba 13, 2023 kuwa sikukuu ya kitaifa ya upanzi wa miti.