Upande wa mashtaka leo uliwasilisha mahakamani mashahidi wa kwanza wawili katika kesi inayomkabili mwendeshaji magari Maxine Wahome ambapo anadaiwa kumuua mpenzi wake Asad Manzour Khan.
Waendesha mashtaka wameratibu mashahidi wengine 17 katika kesi hiyo. Kesi hiyo inasikilizwa na jaji Lilian Mutende.
Shahidi wa kwanza Chemutai Sogomo aliambia mahakama kwamba marehemu Khan na Wahome ambao wote walikuwa washindani wa mbio za uendeshaji magari walikuwa wakizozana kila mara na kwamba siku ya kifo cha Khan alisikia wakivurugana ndani ya nyumba yao.
Sogomo alisema alimfahamisha mlinzi kuhusu vurugu nyumbani kwa wawili hao usiku huo na mlinzi akamwomba aende ajaribu kuwatuliza.
Wahome na Khan walikuwa wanaishi pamoja mtaani Kileleshwa jijini Nairobi na mapigano yao ya siku hiyo yalisababisha Khan kulazwa hospitalini akiwa amepoteza fahamu na baadaye akaaga dunia.
Bi. Maxine alishtakiwa kwa mauaji ya Khan Disemba 12, 2022 akakanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana.
Mawakili wake ni Philip Murgor, Andrew Musangi na Steven Kimathi.