Umoja wa Mataifa waamuru kesi dhidi ya Kabuga isimamishwe

Marion Bosire
2 Min Read

Majaji wa rufaa wa umoja wa mataifa wameamuru kwamba kesi ya makosa ya kivita dhidi ya mshukiwa wa mauaji ya halaiki nchini Rwanda Felicien Kabuga isimamishwe kwa muda usiojulikana kwa sababu anaugua ugonjwa wa matatizo ya kiakili.

Kulingana na majaji hao, Kabuga hastahili hata kushtakiwa kupitia mpango mbadala ambao ni rahisi.

Uamuzi huo uliotolewa jana Jumatatu huenda ukamaanisha kwamba kesi hiyo dhidi ya Kabuga iliyoanza mwaka jana mjini The Hague, haitakamilika.

Mwezi Juni majaji wa mahakama za makosa ya jinai za kimataifa waliamua kwamba Kabuga hafai kushtakiwa lakini anaweza kupitishwa kwa mpango mbadala ambao ni rahisi kidogo kuliko kesi hiyo.

Viongozi wa mashtaka kwa upande wao walikuwa wamesema kwamba kusimamishwa kesi hiyo ni hujuma kwa waathiriwa na ni matendo yake Kabuga yalimweka katika hali hiyo ya kushtakiwa mahakamani wakati umri wake umemzidi na afya yake imedhoofika.

Hata hivyo majaji wa rufaa walisema Jumatatu kwamba mahakama ya chini ilikosea kisheria na hakuna mpango mbadala wa kisheria wa kumshtaki Kabuga kwa nia ya kumhukumu.

Majaji hao walikiri kwamba uamuzi wao huenda ukahuzunisha hata zaidi waathiriwa wa mauaji ya halaiki nchini Rwanda mwaka 1994 ambao wamesubiri muda mrefu kupata haki.

Walielezea kwamba haki inaweza kupatikana tu kupitia kesi zinazoendeshwa kwa njia ya haki na katika kuheshimu haki za washukiwa.

Mahakama ya chini aliamuriwa itafute njia ya haraka ya kumwachilia Kabuga.

Kabuga ambaye alikuwa mwanabiashara na aliyejipatia utajiri kupitia biashara ya majani chai ni mmoja wa washukiwa wa mwisho waliokuwa wakisakwa na mahakama kuhusiana na makosa ya jinai yaliyotekelezwa kwenye mauaji hayo ya halaiki.

Website |  + posts
Share This Article