Waziri wa Afya Susan Nakhumicha amesema serikali imetambua vituo vya afya ambavyo vimekuwa vikiilaghai serikali kupitia Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Matibabu, NHIF.
Kwa mujibu wa Nakhumicha, ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA umeanika uozo uliokithiri wa vituo vya afya kudai malipo ya mabilioni ya fedha kutoka kwa hazima hiyo kupitia ulaghai.
Mathalan, Waziri anasema kati ya mwezi Januari na Disemba 2023, kati ya hospitali 67 zilizokaguliwa, 27 zilibainika kujihusisha katika ulaghai uliosababisha kupotea kwa shilingi milioni 171.
Hospotali hizo hizo zimetakiwa kurejesha fedha hizo na tayari shilingi milioni 17.7 zimerejeshwa huku kukiwa na salio la shilingi milioni 153.3.
Kati ya hospitali 25 zilizohusika, ni 16 ambazo ambazo ama zimerejesha kabisa fedha hizo a sehemu ya fedha hizo.
“Kwa kuelezea hili zaidi kwa kuangazia jumla ya hospitali 8,886, inakadiriwa kuwa hospitali 3,440 huenda zilijihusisha katika ulaghai, yamkini na kusababisha kupotea kwa shilingi bilioni 20 kutoka takriban asilimia 40 zilizojihusisha katika ulaghai. Kwa bahati nzuri, asilimia 60 hazikujihusisha katika uovu huo,” alielezea Nakhumicha.
Kulingana naye, hospitali zilizojihusisha katika ulaghai huo zilitumia mbinu mbalimbali kuilaghai hazina hiyo na kwamba zote zimepigwa marufuku.