Ukosefu wa vyeti vya maadili mema haukubaliki, asema Waziri Kindiki

Martin Mwanje
2 Min Read

Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki ameapa kuangazia suala lisilokubalika la ukosefu wa vyeti vya maadili mema katika Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI. 

Mapema leo Jumatano, Prof. Kindiki alitaarifiwa na timu kutoka DCI ikiongozwa na Mkurugenzi wa idara hiyo Mohamed Amin kuhusiana na hali ilivyo na namna ya kuishughulikia.

“Tumejitolea kuangazia hali ya sasa na isiyokubalika ya ukosefu wa vyeti vya maadili mema katika Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI,” aliahidi Kindiki wakati wa mkutano na maafisa wa DCI.

“Mapema leo asubuhi, nilitaarifiwa na timu ya DCI ikiongozwa na Mkurugenzi Mohamed Amin na kutafakari juu ya uwekaji wa mfumo mpya wa teknolojia ya habari (IT) na kuweka makataa ya kumaliza mrundiko uliopo wa vyeti hivyo ili kurejesha imani ya umma katika utoaji wetu wa huduma.”

Inaonekana Prof. Kindiki ana azima isiyoyumba ya kulainisha utendakazi wa idara zilizopo chini ya Wizara yake.

Katika siku za hivi karibuni, amekuwa akifanya ziara za kushtukiza katika jumba la Nyayo kwa lengo la kulainisha utoaji wa pasipoti kwa wanaozihitaji.

Kwa muda sasa, Wakenya wengi wamekuwa wakilalamikia namna wanavyokawishwa katika kupata stakabadhi hiyo muhimu ya usafiri na wakati mwingine kutakiwa kuwazunguka mbuyu maafisa wa uhamiaji kabla ya kukabidhiwa stakabadhi hiyo.

Prof. Kindiki ameapa kutokomeza ufisadi katika idara hiyo na kuhakikisha maombi ya pasipoti yanashughulikiwa kwa wakati mwafaka.

Share This Article