Juma moja tu baada ya hali mbaya ya barabara ya Ithagani-Ngorika-Kanyiriri katika eneo la Olkalou kaunti ya Nyandarua kuangaziwa na vyombo vya habari, sasa ukarabati wa barabara hiyo umeanza.
Hata hivyo mamlaka ya barabara za vijijini KERRA imefafanua kuwa barabara hiyo iko chini ya usimamizi wa serikali ya kaunti ya Nyandarua kinyume na matamshi ya Gavana Kiarie Badilisha kuwa iko chini ya usimamizi wa KERRA.
Kufuatia ombi la mbunge wa Olkalou Njuguna Kiaraho kwa mamlaka ya Kerra, shirika hilo kupitia waraka uliotiwa sahihi na mhandisi Willy Mburu, limefanua kuwa barabara hiyo iko chini ya usimamizi wa serikali ya kaunti.
Wakaazi wa Ngorika sasa wamekariri umuhimu wa wananchi kuambiwa ukweli ili kuepusha chuki baina ya viongozi.
Wamesema licha ya ukarabati wa barabara hiyo kuanza, sharti wahusika wahakikishe kuwa viungo vinavyotumika ni vya hali ya juu ili kuokoa fedha za uma.
Wakati huo huo wamemtaka naibu wa rais Rigathi Gachagua kuhakikisha kuwa ahadi ya kuweka lami barabara hiyo inatekelezwa ili kufanikisha usafiri wa haraka katika eneo hilo.
Wakulima na wenye magari wamekuwa wakilalamikia hasara kubwa wanayopata kutokana na hali mbaya ya barabara hiyo.
Mbunge wa Olkalou Njuguna Kiaraho amesema kuwa angali anafuatilia serikali kuweka barabara hiyo chini ya mamlaka ya Kerra kwani ina umuhimu mkubwa haswa msongamano unapotokea katika barabara ya Mbaruk-Nakuru.