Ukame wa dhahabu ya mita 10,000 Olimpiki wavuka miaka 56 huku Cheptegei akiwika

Dismas Otuke
1 Min Read

Ni miaka 56 imepita tangu Kenya ijishindie dhahabu ya kwanza ya  mita 10,000  kaitika  michezo ya Olimpiki  iliyotwaliwa na marehemu Naftali Temu.

Yaonekana ukame na subira hiyo huenda ikagonga miongo sita pengine tukifanikiwa mwaka 2028.

Daniel Mateiko,Bernard Kibet na Nicholas Kimeli walikuwa na mtihani mgumu kwenye fainali ya Ijumaa usiku jijini Paris Ufaransa,mikakati na hesabu zao zikionekana kufanya vyema hadi mizunguko 21.

Hata hivyo mambo yalitibuka katika mzunguko wa mwisho wa 24 pale Joshua Cheptegei wa Uganda  alipofyatuka na kushinda dhahabu pekee ambayo ameikosa akiweka rekodi mpya ya Olimpiki.

Mganda huyo ambaye ameshinda dhahabu tatu za Dunia na pia anashikilia rekodi ya dunia, alivuka mstari wa kumalizia kwa dakika 26 sekunde 43.14.

Medali ya fedha ilimwendea Berihu Aregawi wa Ethiopia, huku Mmarekani Grant Fisher akiridhia shaba.

Mkenya bora kwenye fainali hiyo  Kibet aliambulia nafasi ya 5 kwa dakika 26 sekunde 43.98, ukiwa muda bora wa kibinafsi.

Mateiko alifuata katika nafasi ya 11, huku Kimeli akichukua nambari 14.

Share This Article